Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager
imewasili hapa jana (Septemba 5 mwaka huu) saa 11 jioni ikitokea Dakar, Senegal
ambapo ilichelewa kuunganisha ndege, hivyo kuamua kutumia usafiri wa barabara
kwa vile ni karibu na baadaye kupanda kivuko kuingia Banjul badala ya kulala na
kuchukua ndege nyingine siku inayofuata.
Wachezaji wako katika hali nzuri na leo jioni
wanatarajia kufanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Independence ulioko
Bakau ambao utatumika kwa mechi ya kesho. Timu imefikia hoteli ya Seaview
iliyoko kandokando ya Bahari ya Atlantic.
Mechi hiyo itaanza saa 10.30 jioni kwa saa za
hapa ambapo nyumbani Tanzania itakuwa saa 1.30 usiku, na itachezeshwa na
waamuzi kutoka Rwanda Munyemana Hudu. Waamuzi wasaidizi ni Theogene
Ndagijimana, Honore Simba na Issa Kagabo. Kamishna ni Andy Quamie kutoka
Liberia.
Washabiki na vyombo vya habari vya hapa wanaizungumzia
mechi hiyo ambayo ina umuhimu mkubwa kwa pande zote, huku Gambia ikiwa imeita
wachezaji tisa wanaocheza barani Ulaya na Marekani. Gambia ambayo imepata
uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Gambia (GFA) imepania kuhakikisha
haimalizi mechi za mchujo ikiwa na pointi moja tu.
Kwa upande wa Tanzania, Kocha Kim Poulsen amesema
nia ni kuona Stars yenye pointi sita inamaliza katika nafasi ya pili nyuma ya
Ivory Coast ambayo tayari imechukua tiketi pekee ya kucheza raundi ya mwisho
kutoka kundi hili la C.
“Mechi hii ni muhimu kwetu kwa vile tunataka
matokeo mazuri ugenini. Lakini kikubwa ni kuwa matokeo mazuri si tu yatatuweka
katika nafasi ya kuwa wa pili, lakini vilevile yatatusaidia kuongeza pointi
kwenye viwango vya ubora vya FIFA, na kikubwa zaidi hii ni sehemu ya maandalizi
ya sisi kucheza Fainali za Afrika za 2015,” amesema Kim.
Stars inatarajiwa kupangwa hivi; Juma Kaseja,
Vincent Barnabas, Erasto Nyoni, Nadir Haroub, Henry Joseph, Frank Domayo,
Haruni Chanongo, Amri Kiemba, Mrisho Ngasa, Simon Msuva na Khamis Mcha.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF)
+2207362384 Banjul
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni