Ligi kuu soka ya Tanzania bara inataraji kuunguruma
tena hapo kesho kwa kushuhidiwa mchezo mmoja pekee utakaopigwa kwenye uwanja wa
Ally Hassan Mwinyi mjini Tabora ambapo wenyeji wa Rhino Rangers watawakaribisha
wauza mitumba wa Ilala watoto wa jiji Ashanti United.
Timu zote zinashuka dimbani zikiwa tayari
zimeshacheza mechi tano ambazo kwa upande wa wenyeji Rhino rangers zimewawezesha
kuvuna points 4 baada ya kutoka sare michezo minne na kupoteza mmoja wakati kwa
upande wa Ashanti yenyewe imepoteza michezo minne na kutoka sare mmoja uliowapa
alama 1 pekee.
Afisa habari wa Ashanti United Rajab Marijan amesema
kuwa kikosi chao kipo imara kuelekea kwenye mchezo huo licha ya kukabiliwa na
majeruhi akiwemo mkongwe Said Maulid.
“Kiujumla kimaandalizi tuko vizuro japo tuna
matatizo na wachezaji wawili na kwamujibu wa taarifa ya daktari, wachezaji hao
hawatocheza kesho”.
“Mechi za mikoani nguvu ingawaje TFF wakae na
kuangalia upya kutokana na aina ya viwanja tunavyokutana navyo pamoja na
michezo tunayokutana nayo, michezo ya mikoani imejaa fitna na haiangalii usawa”
Marijan ameongezea kuwa bado wananafasi nzuri ya
kupata matokeo mazuri katika mechi zake za nyumbani huku akilitaka shirikisho
la mpira wa miguu nchini TFF kutazama upya viwanja mbalimbali vya mikoani
ambavyo vinatumika katika ligi licha ya kuwa katika ubora unaotakiwa.
“Tumejipanga
kuhakikisha tunashinda dhidi ya Rhino na turudi tukashinde mechi za nyumbani,
kulingana na matokeo ya ligi timu hazijapishana sana kwahiyo matokeo hayatushtui”.
Kwa upande wa Rhino Rangers yenyewe wamesema kuwa
mchezo huo utatumika kuwapa alama tatu muhimu zitazowaweka katika nafasi nzuri
kuelekea kwenye mechi zake zingine za mzunguko wa kwanza wa ligi.
Ligi hiyo itaendelea tena September 28, ambapo
mabingwa watetezi Yanga Afrika baada ya kupoteza mchezo wake uliopita mbele ya
Azam, wanataraji kuzichanga upya karata zao za kutetea ubingwa watakapoikabili
Ruvu shooting katika mchezo utakaopigwa uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.
Huko Tanga katika uwanja wa Mkwakwani Mgambo JKT
watamenyama na JKT Oljoro, Mbeya City wakiwakaribisha wagosi wa kaya Coastal
Union katika uwanja wa Sokoine mjini humo huku Rhino rangers ikitaraji kujitupa
tena kiwanja chake cha nyumbani kucheza dhidi ya Kagera sugar.