Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) anayemaliza muda wake, Leodegar
Tenga amesema amefurahishwa na jinsi kampeni za uchaguzi zinazokwenda kutoka na
ukweli kuwa wagombea wamekuwa wakielezea kile wanachotaka kuufanyia mpira wa
miguu.
Akizungumza
na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF , Rais Tenga ambaye pia ni
mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)
amesema Watanzania wanataka kusikia ajenda za wagombea.
“Ombi
langu ni kwamba kampeni zimeanza vizuri, watu wanazungumza hoja zaidi. Ni
jukumu la wajumbe kupima na kufanya uamuzi. Kwangu mimi nimejitayarisha
kumkabidhi Katiba, Rais mpya wa TFF,” amesema.
Tenga
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki
na Kati (CECAFA) amesema kazi kubwa iliyofanywa na uongozi wake ni kujenga
taasisi (TFF) pamoja na kuweka mifumo (structure) inayoainisha majukumu ya kila
mmoja.
“Ajenda
yetu wakati tunaingia madarakani mwaka 2005 ilikuwa ni kujenga taasisi. Tayari
taasisi ipo, sasa mtazamo uwe kuushughulia mpira wa miguu wenyewe,” amesema.
Mkutano
Mkuu wa TFF unafanyika kesho kwenye ukumbi wa mikutano wa NSSF Waterfront, na
tayari wajumbe wa mkutano huo ambao pia utakuwa na ajenda ya uchaguzi siku
inayofuata wameshawasili jijini Dar es Salaam.
Wawakilishi
kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Ashford Mamelodi
ambaye ni Ofisa Maendeleo wa kanda hii, Magdi Shams El Din ambaye ni mjumbe wa
Kamati ya Utendaji ya CAF na Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) ni
miongoni mwa wageni watakaohudhuria mkutano huo.
Boniface
Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni