REDD’S Miss Tanzania 2012/2013, Brigitte Alfred
ambaye pia alifanikiwa kushika nafasi ya tatu katika shindano la Beauty With a
Purpose wakati wa kuwania taji la dunia (Miss World) mwaka huu, amerejea nchini
na kuwashukuru Watanzania kwa kumuunga mkono kwa kipindi chote alichokuwa
akishikilia taji hilo.
Brigitte alifanikiwa kushika nafasi hiyo katika
shindano hilo, ambalo lilishirikisha warembo zaidi ya 190 kutoka sehemu
mbalimbali duniani, ambalo lilikuwa mahususi kwa warembo kuonyesha kazi
walizofanya kwa jamii katika nchi wanayotoka.
Mrembo huyo alionyesha jinsi alivyosaidia kwa kiasi
kikubwa kutoa msaada kwa watu wenye mahitaji maalumu hasa wale wenye ulemavu wa
ngozi.
Akizungumzia kuhusu shindano la Miss World alisema,
lilikuwa na changamoto nyingi na anaamini ni lazima Watanzania wajivunie
mafanikio ambayo yamefikiwa mpaka sasa katika mashindano hayo ya dunia.
Mafanikio makubwa zaidi ambayo Tanzania iliwahi
kuyapata ni pale Nancy Sumari alipofanikiwa kutwaa taji la Miss World Africa
katika mashindano yaliyofanyika mwaka 2005.
Kuhusu kipindi chote alichokuwa akishikilia taji la
Redds Miss Tanzania alisema, alipata ushirikiano mkubwa na akatoa shukrani kwa
jamii kumuunga mkono kwa kipindi chote hicho.
“Napenda kutoa shukrani za dhati kwa Kamati ya
Redd’s Miss Tanzania, wazazi wangu, vyombo vya habari, Serikali na Watanzania
kwa ujumla kwa kuniunga mkono kwa kipindi chote hicho.
“Kusema kweli sina cha kuwalipa na naahidi
nitaendelea kushirikiana na kamati hii katika kuhakikisha Tanzania inafanya
vyema zaidi katika mashindano ya dunia siku za baadaye,” alisema.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International, Hashim
Lundenga ambao ndio waandaaji wa Redd’s Miss Tanzania alisema, wanajivunia kwa
kiasi kikubwa mafanikio yaliyofikiwa na Brigitte katika mashindano hayo.
“Kwetu tunachukua fursa hii kuyaomba makampuni au
taasisi mbalimbali kujitokeza kudhamini mashindano haya kwani ni muhimu zaidi
kwa ustawi wa Taifa,” alisema.
Taji la Redd’s Miss Tanzania kwa sasa linashikiliwa
na Happiness Watimanywa ambaye alifanikiwa kulitwaa hivi karibuni.
Shindano la Redd’s Miss Tanzania linadhaminiwa na
kinywaji cha Redd’s Original kinachozalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia
Tanzania (TBL).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni