Jumatano, 23 Oktoba 2013

KI MOON: APRM NI NGUZO YA UTAWALA BORA AFRIKA




KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon ameueleza Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) kuwa nguzo muhimu katika kukuza utawala bora barani humo.
Bw. Ki Moon pia amewapongeza viongozi wa nchi za Afrika kwa kubuni na kutekeleza Mpango huo ambao ulianzishwa kutokana na mawazo ya NEPAD katika kuhakikisha kuwa Bara la Afrika linakuwa na utawala bora ili kuchagiza maendeleo.
Bw. Ki Moon alitoa pongezi hizi wiki hii jijini New York alipokutana na viongozi waandamizi wa APRM na NEPAD ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 68 ya UN na Wiki ya Afrika na NEPAD.
Akizungumzia kuhusu APRM, Bw. Ki Moon alisema kwa miaka 10 hii ya mwanzo tangu Mpango huo ulipoanzishwa, Bara la Afrika limeweza kupiga hatua kwani mchakato huo unahimiza utawala bora, kuheshimu katiba na kupanua demokrasia.
“APRM imeweza kusaidia kuweka utamaduni wa kisiasa wa kuheshimu utawala bora miongoni mwa Serikali za Afrika. Mchakato huu umeweza kuweka hadharani kanuni za kidemokrasia za kufuatwa na kuhimiza katika mijadala kukabiliana na migogoro,” alisema.
Tanzania ni miongoni mwa nchi 33 kati ya 54 za Umoja wa Afrika (AU) zilizojiunga na APRM na tayari imekamilisha Ripoti yake ya kujitathmini inayoonesha hali ya utawala bora nchini.
Bw. Ki Moon alitumia wasaa huo pia kuzipongeza nchi 17 zilizokwishakamilisha Ripoti zao za kujitathmini. Tanzania na Zambia zilitathminiwa Januari mwaka huu hivyo kufikisha idadi ya nchi hizo 17 kati ya 33.
 “Nazipongeza nchi 17 zilizohitimisha tathmini ya mwanzo. Mchakato huu umeweza kuimarisha uwajibikaji wa ndani ya nchi husika. Katika baadhi ya maeneo APRM imeweza hata kuainisha viashiria vya migogoro na kutoa mapendekezo juu ya namna ya kuitatua,” aliongeza.
Kutokana na thamani ya mchakato wa APRM, Bw. Ki Moon licha ya kutaka Mpango huo uimarishwe zaidi, alizitaka nchi wahisani na jumuiya ya kimataifa kuendelea kuupa msaada Mpango huo ili ufanikishe malengo yake. Mwaka huu APRM imetimiza miaka 10.
“Miaka 10 iliyopita APRM ilianzishwa ikiwa ni mchakato wa kijasiri ulioionesha dunia kuwa Afrika iko tayari kuchukua hatua za kukabiliana na na changamoto mbalimbali inazokutana nazo katika ujenzi wa demokrasia.
“Miaka kumi sasa, Mpango huu umethibitisha thamanai yake. Katika kuadhimisha hili naziomba jumuiya za kimataifa kuzisaidia NEPAD na APRM. Tuzisaidie kufikia hatua ambapo viongozi wa Afrika watakuwa wakizidi kuwajibika kwa watu wao na kwa njia za kidemokrasia zaidi,” alisisitiza.
APRM ilianzishwa Machi 9, 2003 ikiwa na lengo la kufanya tathmini za mara kwa mara za utawala bora miongoni mwa nchi wananchama kwa lengo la kubaini changamoto za kufanyiwakazi na mambo mazuri ya kuimarishwa au kuigwa na nchi nyingine.
Tanzania ilijiunga na Mpango huu mwaka 2004, Bunge likaridhia APRM kuanza kazi nchini mwaka 2005. Januari mwaka huu Rais Jaakaya Kikwete aliiwasilisha na kuitetea Ripoti ya Tanzania mbele ya Wakuu wenzake wa Nchi na Serikali za APRM mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni