HOTUBA
YA ATHUMANI JUMANNE NYAMLANI KWENYE MKUTANO WAKE NA WAANDISHI WA HABARI ALHAMIS
TAREHE 24 OKTOBA 2013
Ndugu
waandishi, Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwenu nyinyi
binafsi na vyombo vyenu vya habari kwani ni kweli kwamba mmeacha kazi nyingi na
za muhimu na kunipa nafasi ya kuongea nanyi siku ya leo.
Nasema Ahasanteni sana.
Ndugu
waandishi, Wito wangu kwenu hapa ni kutaka kuongea na
watanzania wenzenu kupitia ninyi ambao kwa imani yangu nyinyi ndio kiunganishi
kikubwa cha jamii. Napenda kuongelea kuhusu nia yangu niliyoionesha ya kugombea
nafasi ya Rais wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania – TFF. Bila ya
kuwapotezea muda naomba nianze kwa kukiri kwenu kuwa uamuzi wangu huu haukuwa
rahisi kwasababu nafahamu majukumu mazito ambayo yanatakiwa kutekelezwa na Rais
wa shirikisho la mpira wa miguu hasa kwa nchi kama yetu ambayo imekuwa
ikikumbwa na changamoto mbalimbali katika uendelezaji wa michezo hasa wa soka.
Ndugu
waandishi, wote wanafahamu kuwa nimekuwa kiongozi wa mpira wa
miguu kwa muda mrefu sasa, katika ngazi mbalimbali kama inavyooneshwa katika
kikaratasi changu chenye maelezo yangu mafupi nilichosambaza. Kwa hivi sasa ni
makamu wa kwanza wa Rais wa shirikisho la mpira wa miguu nafasi ambayo nimekuwa
nayo kwa takribani miaka minne sasa
nikiwa kama msaidizi mkuu wa mheshimiwa Leodger Chilla Tenga ambaye ni Rais wa shirikisho
anayemaliza muda wake.
Ndugu
waandishi, Ni kweli usiofichika kwamba katika kipindi cha
uongozi wa mheshimiwa Tenga ambaye mimi nilikuwa msaidizi wake mkuu, tumepata
mafanikio makubwa yakiwemo kujenga mfumo imara wa uendeshaji wa soka nchini kwa
kuimarisha menejimenti ya soka, kuimarisha ligi kuu pamoja na ligi nyingine na
kuimarisha timu za taifa. Mafanikio haya yaliongeza uaminifu wa shirikisho kwa
wadhamini na wafadhili mbalimbali wa mashindano yetu nah ii yote ni kazi ya
uongozi wa mheshimiwa Tenga.
Ndugu
waandishi, Hakuna kazi yoyote inayoleta mafanikio bila kuwa
na changamoto zake na nikiri kwamba tulikutana na changamoto mbalimbali katika
utekelezaji wa majukumu yetu jambo ambalo kwa kiasi kikubwa ndilo lililonifanya
niamue leo kufanya uamuzi huu mgumu kwa kuamua kuomba ridhaa ya watanzania
kuongoza shirikisho hili kwasababu nazijua vyema changamoto hizi ambazo
zimekuwa zikiukumba mchezo wa soka nchini na hivyo nitakuwa sijatenda haki kwa
nafsi yangu, mchezo wa soka na taifa langu kwa kuwa mbinafsi kiasi hili cha
kuamua kutogombea na hivyo kushindwa kutumia uzoefu wangu katika kuendeleza
mafanikio tuliyoyapata na kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza na
zitakazojitokeza.
Ndugu
waandishi, Sote tunafahamu kuwa ni hamu ya wapenzi
na mashabiki wa soka nchini kuona kuwa tunapata mafanikio ya haraka katika soka
hasa kwa kuzingatia uwekezaji tulioweka katika soka kwa kipindi cha takribani
miaka nane sasa hasa suala la timu za taifa kushiriki katika mashindano ya
kimataifa kama vile mashindano ya kombe la mataifa Afrika na kombe la Dunia
jambo ambalo kwa maoni yangu na uzoefu wangu tunakaribia kulifikia na kama
nitapata ridhaa ya watanzania (wajumbe wa mkutano mkuu) nitatekeleza mambo
makuu tisa (9) ambayo ni:
1.
Kuimarisha
usimamizi na menejiment ya soka katika ngazi zote
2.
Rushwa
katika soka nchini
3.
Kukuza
soka la watoto, vijana na wanawake
4.
Kuimarisha
uwezo wa rasilimali fedha wa shirikisho
5.
Kuongeza
idadi na ubora wa waamuzi, walimu wa soka na wataalamu wa Afya ya michezo
6.
Kuongeza
ubora ligi kuu, ligi daraja la kwanza, ligi za wilaya na mikoa
7.
Kuongeza
idadi ya mawakala wa wachezaji ambao ni watanzania
8.
Kuimarisha
ushirikiano wa TFF na serikali
9.
Kuimarisha
Ushirikiano wa TFF, CAF na FIFA.
Ndugu
waandishi, Maeneo hayo tisa niliyokutajia hapo juu kwa ujumla
wake kwa uzoefu wangu katika soka la Tanzania na Afrika yatasaidia kutatua
changamoto mbalimbali tunazokumbana nazo mathalani ukuzaji wa soka la vijana
kwaajili ya kuzalisha wachezaji wengi wenye uwezo wa kushindana na ambao
wanaweza kukaa pamoja kwa muda mrefu.
Ndugu waandishi, Nawashukuru sana
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni