Na. Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya
Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, Salum Bausi amewaita nyota 30 kuunda kikosi cha
timu hiyo kinachojiandaa na michuano ya Chalenji inayotarajiwa kuanza kutimua
vumbi mjini Nairobi Kenya baadae mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari
katika ukumbi wa mikutano wa uwanja wa Amaan mjini hapa, Bausi alisema pamoja
na kuwaona wachezaji wengi katika ligi madaraja tofauti ya hapa Zanzibar na
wale wanaoshiriki ligi kuu ya Tanzania bara, amezingatia mambo makubwa manne
ili kuipata timu hiyo.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni
nidhamu ya mchezaji, uwezo wa mchezaji binafsi, nafasi ya mchezaji katika timu
yake na ukubwa wa mashindano wanayojiandaa nayo jambo ambalo amesema litawapa
nafasi wachezaji hao kuongeza juhudi na kujituma wakiwa katika timu hiyo.
“Pamoja na mambo yote hayo mkazo mkubwa kwangu
ni katika nidhamu ya mchezaji, ndani na nje ya uwanja kwani naamini ni vigumu
kama mwalimu kuwa na timu yenye matokeo mazuri bila ya wachezaji wanaozingatia
nidhamu wakati wote”, alisema Bausi.
Bausi ambaye awali alitangaza
kujiuzulu timu kuifundisha timu hiyo mara baada ya kushika nafasi ya tatu
katika mashindano yaliyopita yaliyofanyika Kampala, Uganda na alirudishiwa
jukumu hilo na ZFA (chama cha soka Zanzibar) baada ya kushauriwa wa Rais wa
Zanzibar Dk. Ali mohammed Shein.
Aliwataka wadau wa mchezo huo
kujitokeza na kumpa ushirikiano na kwamba yeye atakua tayari kupokea ushauri
wowote ule.
“Hii timu hii si yangu wala ZFA ni
yetu sote, sasa kila mmoja anaruhusiwa kutoa mchango, maoni, ushauri na kila
aina ya msaada ambao anahisi utasaidia katika kuleta matokeo mazuri ya timu
hii”, aliongeza.
Wachezaji watakaounda timu hiyo na
timu zao kwenye mabano ni walinda milango Mwadini Ali Mwadini (Azam fc),
Abdalla Rashid ‘Babu’ (Ruvu Shooting) na Ali Suleiman Abdi (KMKM) wakati
walinzi ni Mohammed Azan ‘Brown’ (Polisi - Zanzibar), Waziri Salum (Azam ),
Shafii Hassan (Malindi) na Mohammed Faki (Zimamoto).
Wengine katika nafasi hiyo ni Salum
Haji Juma (Miembeni), Said Yussuf (Mtende Rangers), Mohammed Othman Mmanga
(Jamhuri), Mussa Said Magarawa (Chwaka Stars) na Nassor Masoud ‘Cholo’ (Simba).
Viungo wa timu hiyo ni pamoja na
Abdulhalim Humuod (Simba), Sabri Ali Makame (Oljoro JKT), Adeyoum Saleh (Simba)
na Is-haka Othman (JKU).
Wengine ni Ali Kani Mkanga (JKT
Ruvu), Hamadi Mshamata (Chuoni), Hamadi Juma Issa na Masoud Ali Mohammed
(Mtibwa Sugar).
Washambuliaji katika kikosi hicho
kinachotarajiwa kuanza mazoezi Alhamisi ijayo baada ya kukamilika kwa zoezi la
upimaji wa afya siku ya Jumatano ni Seif Abdalla Rashid na Khamis Mcha Khamis
‘Viali’ wa Azam, Suleiman Kassim Suleiman ‘Solembe’ (Coastal Union), Amour Omar
Mohammed ‘Janja’ (Miembeni) na Amir Omar Hamad (Oljoro JKT).
Wachezaji wengine katika safu ya
ushambuliaji ni Jaku Joma Jaku (Mafunzo), Faki Nahoda (Kimbunga F. C), Hassan
Seif Ali (Mtibwa) na mfungaji bora wa mashindano ya kombe copa cola
yaliyomalizika hivi karibuni Juma Ali Yussuf anaechezea timu ya New Vission
inayoshiriki ligi daraja la central wilaya ya Mjini, Unguja.
Akizungumzia uteuzi huo mjumbe wa
Kamati Tendaji ya ZFA Taifa Maalim Masoud Attai aliwataka wapenzi wa mpira wa
miguu visiwani hapa wakubaliane nao kutokana na kuwa umezingatia vigezo vya
kitaaluma na waisaidie ili kuwatia moyo wachezaji na viongozi wa timu hiyo.
“Huu ni uteuzi wa mwalimu na
wenzake na sisi sote hatuna budi kuunga mkono kwa sababu wao ndio tuliwakabidhi
kazi hivyo ni vyema tukawasaidia kutekeleza majukumu yao”, alisema Maalim
Attai.
Timu hiyo ambayo inatarajiwa
kucheza mechi mbali mbali za mchujo ili kupata wachezaji 20 watakaoenda
Nairobi, ipo chini ya Bausi anayesaidiwa na Hafidh Muhidin na Malale Hamsini
huku Saleh Ahmed Seif akipewa jukumu la kuwanoa makipa wa timu hiyo na daktari
wa timu ni Mohammed Mwinyi na mtunza vifaa ( kit manager) ni Mohammed Said
‘Mdudu’.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni