Ofisi ya Taifa ya
Takwimu, Wizara ya Fedha ina jukumu la kukokotoa Pato la Taifa kwa robo Mwaka
ili kuwapatia takwimu kwa wakati, wadau wa takwimu za Pato la Taifa
katika vipindi vifupi vya robo mwaka ili kuweza kutathmini mabadiliko ya ukuaji
wa uchumi.
Ukuaji halisi wa
Pato la Taifa la Tanzania kwa bei za soko uliongezeka kwa kasi ya asilimia 6.7
katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013 ikilinganishwa na kasi ya
asilimia 6.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2012. Jumla ya thamani ya Pato la
Taifa katika kipindi husika ilikuwa Shilingi 5,012,935 milioni mwaka 2013
ikilinganishwa na Shilingi 4,699,884 milioni mwaka 2012.
Ukuaji wa Shughuli
za Uchumi za Kilimo na Uvuvi
Shughuli za
kiuchumi za kilimo zilifikia kasi ya ukuaji ya asilimia 5.3 katika kipindi cha
robo ya pili ya mwaka 2013 zikilinganishwa na asilimia 5.1 ya robo kama hiyo
mwaka 2012. Katika kipindi hicho, kulikuwa na mvua za kutosha katika mikoa
inayozalisha mazao kwa wingi. Aidha, maelekezo ya ma-ofisa Ugani kwa wakulima
kama kuchagua aina bora ya mbegu yalisaidia kuongeza uzalishaji.
Shughuli za uvuvi
zilifikia kasi ya ukuaji wa asilimia 2.4 katika robo ya pili ya mwaka 2013
ikilinganishwa na asilimia 6.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2012. Kasi ya ukuaji huu ilipugua
kutokana na kupungua kwa mavuno ya samaki kutoka kwenye maziwa, mito na
mabwawa.
Shughuli za Uchumi za Viwanda na Ujenzi
Shughuli za uchimbaji madini, mawe na kokoto ziliongezeka kwa kasi ya
asilimia 4.3 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013 ikilinganishwa na
kuporomoka kwa kasi ya ukuaji wa asilimia 5.1 katika kipindi kama hicho mwaka
2012. Kuongezeka kwa kasi hii ya ukuaji ilitokana na kuongezeka kwa uzalishaji
wa madini ya almasi na Tanzanite katika robo ya pili ya mwaka 2013.
Shughuli za uzalishaji bidhaa viwandani zilifikia kasi ya ukuaji ya
asilimia 5.8 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013 ikilinganishwa na
kasi ya asilimia 8.2 mwaka 2012. Kupungua kwa kasi ya ukuaji ya asilimia 2.4
(percentage point) kulitokana na kupungua kwa uzalishaji wa sementi, vyakula
vilivyosindikwa na nguo.
Uzalishaji wa nishati ya umeme ulifikia kasi ya ukuaji wa asilimia 4.5
katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013 ikilinganishwa na kuporomoka kwa
kasi ya ukuaji ya asilimia 1.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2012. Kuongezeka
kwa ukuaji wa nishati ya umeme kwa asilimia 5.6 (percentage point) kulitokana
na kuongezeka kwa uzalishaji wa nishati ya umeme unaotokana na mafuta na
gesi.
Ukuaji wa Shughuli za Uchumi za Utoaji Huduma
Shughuli za biashara za jumla na reja reja, ukarabati wa magari na
pikipiki na vifaa vingine vya majumbani zilifikia kasi ya ukuaji wa asilimia
5.9 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013 ikilinganishwa na kasi ya
asilimia 7.0 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2012. Kupungua kwa kasi
kwa asilimia 1.1 (percentage point) kulitokana na kupungua kwa bidhaa
zilizotengenezwa hapa nchini na zilizoagizwa kutoka nje ya nchi zilizouzwa
katika kipindi hicho. Shughuli za upangishaji nyumba, na shughuli zingine
za biashara zilifikia kasi ya ukuaji wa asilimia 6.7.
Shughuli za uchukuzi na mawasiliano zilifikia kasi ya ukuaji wa asilimia
14.8 katika kipindi husika. Shughuli nyingine ni huduma za Hoteli na migahawa
zilizofikia kasi ya ukuaji wa asilimia 3.2; Shughuli za uendeshaji Serikali
zilifikia kasi ya asilimia 5.0, Elimu asilimia 5.7 na huduma za Afya na
shughuli nyinginezo zilifikia kasi ya ukuaji wa asilimia 3.8 katika kipindi
hicho.
Imetolewa na:
Morrice Oyuke
Mkurugenzi wa Takwimu za Kiuchumi
Ofisi ya Taifa ya Takwimu
Dar es Salaam
Kwa mawasiliano zaidi kuhusu Takwimu za Pato la Taifa kwa robo ya pili ya
mwaka 2013, wasiliana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwenye anuani
zifuatazo:
Mkurugenzi kuu,
Ofisi ya Taifa ya Takwimu,
S.L.P. 796, Dar es Salaam.
Simu: +255 22 212 2722/3/4
Nukushi: +255 22 2130852
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni