Mlinda mlango wa mabingwa wapya wa ligi kuu soka ya
nchini Kenya Gor Mahia Ivo Philip Mapunda,amesema kuwa kila kitu kinawezekana kwasasa
baada ya kupata nafasi kurejea kwenye timu yake ya Taifa ya Tanzania bara baada
ya kuwa nje kwa muda mrefu.
Kipa huyo kujumuishwa kwenye timu ya taifa ya
Tanzania bara The Kilimanjaro Stars ambayo inajiandaa na michuano ya Chalenj
itakayofanyika nchini Kenya kumezua mshangao mkubwa miongoni mwa mashabiki
mbalimbali wa soka waliopo Kenya na Tanzania.
Mapunda ambaye ni mahiri kupangua mikwaju ya penalty
amejumuishwa katika kikosi cha wachezaji 30 ambao watafanyiwa mchujo na kubakia
wachezaji 10 watakaoungana na kikosi cha kwanza cha The Kilimanjaro Stars.
Mapunda amesema haijalishi yeye kuitwa kikosi cha
kwanza au cha pili kikubwa ni kuonekana kwenye kikosi hicho ambacho kwa muda
mrefu hajakitumikia na ameahidi kufanya jitihada zake kuhakikisha wanarejea na
kikombe nyumbani Tanzania.
Michuano ya Chalenj inataraji kutimua vumbi kuanzia
Novemba 27 hadi Disemba 12 mwaka huu na kipa huyo tegemezi wa Gor Mahia
ataungana na makipa wengine akiwemo Aishi Manula kutoka Azam na Hussein Sharif
kutoka Mtibwa katika kikosi kitakachofanyiwa na mchujo kabla ya kuungana na
mlinda mlango namba moja wa Yanga Afrika Ally Mustapha Mtinge Barthez katika
kikosi kamili kitakacho kwea pipa kuelekea Nairobi nchini Kenya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni