Katibu mkuu wa mabingwa wapya wa ligi kuu soka
nchini Kenya George Bwana ameukata mzizi wa fitna na kubainisha wazi kocha wao
aliowapa ubingwa msimu huu Bobby Williamson haendi popote bado na wataendelea
kuwa nae kwa misimu mingine ijayo.
Saa 24 zilizopita Kocha huyo wa zamani wa timu ya
taifa ya Uganda amekuwa akihusishwa na taarifa za kuja kuinoa timu kutoka
nyumbani Tanzania ambao ni mabingwa wa zamani wa ligi kuu soka ya Tanzania bara
wekundu wa msimbazi Simba.
Bwana amekiri kumalizika kwa mkataba wa mwaka mmoja
wa kocha huyo pamoja na mambo mengine amebainisha maamuzi ya klabu kumuongezea
mkataba mwingine kuelekea kwenye msimu ujao wa ligi nchini humo.
Bwana ameongezea kuwa yote yanayoandikwa kwenye
vyombo mbalimbali vya habari vya Tanzania kuhusiana na kocha huyo ni maneno tu
yenye lengo la kuwavuruga.
Kama itakumbukwa hapo jana wakati wakikabidhiwa
ubingwa wao wa ligi msimu huu, kocha wa Gor Mahia Bobby Williamson aliamua
kumzawadia medali yake Patrick Osewe ambaye ni dereva wa gari linalotumika
kubeba kikosi cha Gor Mahia.
Bobby amesema kuwa dereva huyo ni sehemu ya ushindi
walioupata hivyo ana kila sababu ya yeye kujivunia kazi kubwa ya kuwafikisha
salama dimbani ambako wanakwenda kuchukua alama 3 muhimu zilizowaweka kileleni.
Gor Mahia rasmi walizawadiwa kikombe chao cha
ubingwa wa ligi msimu huu mara baada ya kumalizika kwa mchezo wao wa raundi ya
29 ambapo walikubali kichapo cha magoli 2-0 toka kwa KCB.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni