Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa Sayari, Fatuma Bahau ‘Crouch’
kilichotokea jana (Novemba 15 mwaka huu) kwenye Hospitali ya Temeke, Dar es
Salaam.
Msiba huo ni mkubwa katika mpira wa miguu kwani
Fatuma ndiyo kwanza alikuwa anachipukia katika mpira wa miguu wa wanawake
ambapo alikuwa mfungaji bora wa michuano ya U15 Copa Coca-Cola ya mwaka huu
akichezea timu ya Ilala, hivyo mchango wake katika mchezo huu tutaukumbuka
daima.
Kwa mujibu wa mlezi wa mchezaji huyo, Stephania
Kabumba, marehemu anasafirishwa kesho kwenda kwao Mwanza kwa ajili ya maziko
ambapo kifo chake kimesababishwa na ugonjwa wa malaria.
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Bahau,
klabu ya Sayari, Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA) na Chama
cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kuwataka kuwa na subira na
uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Mungu aiweke roho ya marehemu Fatuma mahali pema
peponi. Amina
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni