KAMATI ya Kusimamia Tuzo za
Wanamichezo Bora Tanzania zinazotolewa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo
Tanzania (TASWA) ilikutana Dar es Salaam juzi na kukubaliana masuala mbalimbali
juu ya kuboresha tuzo hizo.
- Tarehe ya Tuzo
Kamati imepanga kuwa tuzo hizo
zifanyike Juni 27, 2014 jijini Dar es Salaam katika ukumbi utakaotangazwa kwa
ushirikiano wa Kamati ya Tuzo na Kamati ya Utendaji ya TASWA.
Tayari Kamati ya Tuzo na Kamati ya
utendaji ya TASWA, zimeanza juhudi za pamoja za kuzungumza na wadhamini
mbalimbali wakubwa na wadogo kwa nia ya kufanikisha tuzo hizo katika tarehe
iliyopangwa na kuna muelekeo mzuri kuhusiana na suala hilo.
- Watakaopewa Tuzo
Kamati yetu kwanza inawaomba radhi
viongozi wa vyama vyote vya michezo kutokana na tuzo kushindwa kufanyika mwaka
jana na hilo kwa mujibu wa taarifa ya uongozi wa TASWA iliyowasilishwa kwenye
kikao chetu, ilitokana na sababu mbalimbali lakini kubwa ni kujitoa dakika za
mwisho kwa baadhi ya kampuni zilizokuwa zimethibitisha kudhamini tuzo hizo.
Hata hivyo tunawaomba tuendelee
kushirikiana nao mwaka huu na kwa kuanzia tutawatumia barua rasmi za kuomba
majina ya wanamichezo wao waliofanya vizuri kuanzia Januari 2013 hadi Aprili
mwaka huu, ambapo matarajio yetu wanamichezo wasiopungua 40 watapewa tuzo.
- Ujumbe wa Tuzo
Pia kamati imeamua kwamba kila mwaka
tuzo hizo zitakuwa na ujumbe maalum kwa wanamichezo, ambapo kwa kuanzia tuzo za
mwaka huu ujumbe wake utakuwa ni: ‘Wanamichezo Tupige Vita Ujangili’.
Tunaamini wale wote wataowania, wale
watakaoshinda tuzo hizo na wanamichezo wote wakiwemo waandishi wa habari za
michezo tutashirikiana na jamii kwa ujumla kwa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha
vita dhidi ya ujangili kwa namna tutakavyomudu.
Pia katika kuhakikisha tuzo za mwaka
huu zinakuwa bora kwa maslahi ya wanamichezo wote hapa nchini, kamati imeteua
baadhi ya viongozi wa kiserikali kuwa washauri wa kamati katika masuala
mbalimbali na sasa tunasubiri majibu yao ili tuweze kuwatangaza rasmi.
Nawasilisha
Rehure Nyaulawa
Mwenyekiti Kamati ya Tuzo
26/03/2014
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni