Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
tumepokea amri ya Mahakama Kuu (Kitengo cha Kazi) kukamata sh. milioni 106 za klabu
ya Yanga kutokana na mapato ya mlangoni kwenye mechi zake ili kuwalipa
waliokuwa wachezaji wake Stephen Malashi na Wisdom Ndlovu.
Tayari tumeanza utekelezaji wa amri hiyo ambapo
katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) dhidi ya Rhino Rangers iliyochezwa
Machi 22 mwaka huu mjini Tabora tumezuia sh. 9,221,250 ambazo ndizo zilizokuwa
mgawo wa Yanga katika mchezo huo ulioingiza jumla ya sh. 38,655,000.
Wachezaji hao walifungua kesi kortini kupinga
mikataba yao na klabu hiyo kuvunjwa bila kulipwa haki zao za kimkataba. Malashi
na Ndlovu walishinda kesi hiyo, hivyo korti kuwapa tuzo hiyo ya sh. milioni
106.
Tunawakumbusha wanachama wetu (klabu za Ligi Kuu,
vyama vya mpira wa miguu vya mikoa na vyama shiriki) kuzingatia mikataba
wanayoingia na watendaji wao wakiwemo wachezaji, makocha na maofisa wengine.
Iwapo wanataka kuvunja mikataba ya ajira wafuate
taratibu kwa vile hakuna mkataba ambao hauelezi jinsi ya kuvunjwa iwapo upande
mmoja unataka kufanya hivyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni