Jumatano, 26 Machi 2014

YANGA YAZIDI KUJIKITA KILELENI


 Vinara wa ligi kuu soka ya Tanzania bara waoka mikate wa Azam fc wamezidi kujikita kileleni mwa ligi hiyo wakifikisha alama 50 baada ya kuwatandika mgambo Jkt mabao 2-0 huko kwenye uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Hadi mapumziko milango ya timu zote ilikuwa migumu na iliwachukua Azam dakika 15 za kipindi cha pili kupata bao la kuongoza kupitia kwa mshambuliaji wake John Bocco Adebayor kabla ya Brian Umony kutumbukia tena wavuni na kuyafanya matokeo ya mchezo huo kumalizika kwa Azam kupata ushindi wa mabao 2-0.

Kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam nao mabingwa watetezi Dar es salaam Young Africans ilikuwa dimbani kukipiga dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons Wajelajela kutoka mjini Mbeya.

Yanga wamefanikiwa kuchomoza na ushindi mnono wa mabao 5-0 mabao yaliyotupiwa wavuni na Emmanuel Okwi dakika ya 20, Mrisho Khalfan Ngassa dakika ya 37, Hamisi Kiiza dakika ya 68, 88 na Nadir Haroub Ally Canavaro dakika ya 78.

Kwa matokeo hayo Yanga wanaendelea kusalia kwenye nafasi ya pili wakifikisha alama 46 wakiwa na mchezo mmoja mkononi.

TUZO ZA TASWA KUFANYIKA JUNE 27 MWAKA HUU


KAMATI ya Kusimamia Tuzo za Wanamichezo Bora Tanzania zinazotolewa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) ilikutana Dar es Salaam juzi na kukubaliana masuala mbalimbali juu ya kuboresha tuzo hizo.

  1. Tarehe ya Tuzo

Kamati imepanga kuwa tuzo hizo zifanyike Juni 27, 2014 jijini Dar es Salaam katika ukumbi utakaotangazwa kwa ushirikiano wa Kamati ya Tuzo na Kamati ya Utendaji ya TASWA.

Tayari Kamati ya Tuzo na Kamati ya utendaji ya TASWA, zimeanza juhudi za pamoja za kuzungumza na wadhamini mbalimbali wakubwa na wadogo kwa nia ya kufanikisha tuzo hizo katika tarehe iliyopangwa na kuna muelekeo mzuri kuhusiana na suala hilo.

  1.  Watakaopewa Tuzo

Kamati yetu kwanza inawaomba radhi viongozi wa vyama vyote vya michezo kutokana na tuzo kushindwa kufanyika mwaka jana na hilo kwa mujibu wa taarifa ya uongozi wa TASWA iliyowasilishwa kwenye kikao chetu, ilitokana na sababu mbalimbali lakini kubwa ni kujitoa dakika za mwisho kwa baadhi ya kampuni zilizokuwa zimethibitisha kudhamini tuzo hizo.

Hata hivyo tunawaomba tuendelee kushirikiana nao mwaka huu na kwa kuanzia tutawatumia barua rasmi za kuomba majina ya wanamichezo wao waliofanya vizuri kuanzia Januari 2013 hadi Aprili mwaka huu, ambapo matarajio yetu wanamichezo wasiopungua 40 watapewa tuzo.

  1. Ujumbe wa Tuzo

Pia kamati imeamua kwamba kila mwaka tuzo hizo zitakuwa na ujumbe maalum kwa wanamichezo, ambapo kwa kuanzia tuzo za mwaka huu ujumbe wake utakuwa ni: ‘Wanamichezo Tupige Vita Ujangili’.

Tunaamini wale wote wataowania, wale watakaoshinda tuzo hizo na wanamichezo wote wakiwemo waandishi wa habari za michezo tutashirikiana na jamii kwa ujumla kwa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha vita dhidi ya ujangili kwa namna tutakavyomudu.

Pia katika kuhakikisha tuzo za mwaka huu zinakuwa bora kwa maslahi ya wanamichezo wote hapa nchini, kamati imeteua baadhi ya viongozi wa kiserikali kuwa washauri wa kamati katika masuala mbalimbali na sasa tunasubiri majibu yao ili tuweze kuwatangaza rasmi.

Nawasilisha

 Rehure Nyaulawa
Mwenyekiti Kamati ya Tuzo
26/03/2014